Mashindano ya kumtafuta Miss Tabata 2010 yatafanyika Mei 28 katika ukumbi wa Dar West Park, Tabata, waandaaji wa mashindano hayo Bob Entertainment na Keen Arts wametangaza jana.
Mratibu wa mashindano hilo Godfrey Kalinga amesema warembo 25 watashindania taji hilo ambalo linashikiliwa na Everlyne Gamasa.
Kalinga alisema warembo 18 wanaendelea na mazoezi katika ukumbi wa Dar West Park kila siku chini ya wakufunzi wawili – Rehema Uzuia na Stella Solomon.
“Tunahitaji warembo wenye sifa waendelee kujitokeza ili tuwe na upinzani wa kutosha. Bado hatujafunga zoezi la usajili,” Kalinga alisema.
Aliwataja warembo wanaoendelea na mazoezi kuwa ni Grace Johannes (18), Anna Mwakapala (18), Consolata Lukosi (20), Happy Emmanuel (20) na Ryhinna Jesse (21).
Wengine ni Harriet Mulumba (20), Benardina Mwita (18), Dorine Deus (18), Light Mziray (20), Roselinne Sekwao (19), Bellynda Mselewa (20), Maria Joseph (18), Lilian Andrew (19), Alice Kidika (23), Grace Mzamiri (23),
Joyce Joseph Sadiki (21), Rose Anthony (23) na Agatha Killala (20).
Kalinga alisema watafanya mchujo mwezi ujao kabla warembo kutembelea mbuga za wanyama Mikumi. “Mchujo itawakumba wale ambao hawana nidhamu na watoro,” alisema mratibu huyo.
Miss Tabata itatumika kuzindua shindano la Vodacom Miss Tanzania mwaka huu.
Warembo zaidi ya 10 watafuzu kushiriki kwenye mashindano ya kanda ya Ilala na baadaye Vodacom Miss Tanzania.
Shindano la Tabata ni moja ya vitongoji viwili vilivyobakizwa kwenye kanda ya Ilala baada ya vingine vitatu kufutwa na waandaaji wa taifa.
Miss Tabata namba mbili wa mwaka jana Julieth William ndiye Vodacom Miss Tanzania namba tatu kwa sasa.
Kalinga alisema kuwa hivi punde wataandaa sherehe maalum katika ukumbi wa Savanna Lounge ulioko kwenye jingo la Mkapa Towers kutangaza wadhamini na kutambulisha warembo.